DOI: 10.51317/ecjkisw.v3i1.205 Volume: 03 Issue: 01 | Feb-2021| Received: 24.01.2021; Accepted 28.01.2021; Published on 28.02.2021 at www.editoncpublishing.org Akaka, L., et al., Editon Cons. J. Kiswahili., Double –Blind Peer Reviewed Journal 211 © 2021, Editon Consortium Publishing | This work is licensed under a Creative Commons Attribution-Non Commercial-Share Alike 4.0 International License. | Website: www.editoncpublishing.org Editon Consortium Journal of Kiswahili (ECJKISW) ISSN: 2663-9289 MAUDHUI KATIKA BEMBELEZI ZA WANAWAKE WATIKUU NCHINI KENYA Lina Akaka1; Sheila Wandera- Simwa2; James Ogola Onyango3 1.2.3 Laikipia University, Kenya Main author email: akakalina2016@gmail.com ---------------------------------------------------------------------***--------------------------------------------------------------------- How to cite this article in APA Akaka, L., Wandera-Simwa, S., & Ogola, J. O. (2021). Maudhui Katika Bembelezi za Wanawake Watikuu Nchini Kenya. Editon Cons. J. Kiswahili, 3(1), 211-222. https://doi.org/10.51317/ecjkisw.v3i1.205 ---------------------------------------------------------------------***--------------------------------------------------------------------- IKISIRI Madhumuni ya makala haya ni kujadili maudhui yanayojitokeza katika bembelezi za wanawake Watikuu nchini Kenya ili kutambua ujumbe uliyomo. Kwa muda mrefu, kitanzu cha bembelezi cha nyimbo za watoto kimepuuzwa miongoni mwa watafiti nchini Kenya na barani Afrika kuna tafiti chache za kitanzu hiki zinazojulikana na watafiti. Bembelezi za wanawake Watikuu zina maudhui ya kipekee yanayotilia shaka hadhira yake na hili ndilo jambo lililowavutia waandishi wa makala haya kuzitafiti na kujadili maudhui yaliyomo. Utafiti wa awali uliofanywa na waandishi ulionyesha kwamba lugha inayotumiwa kuwasilisha ujumbe uliyomo ina urejelezi, kejeli na mafumbo chungu nzima ambayo ni kinyume cha sifa za lugha ya nyimbo za watoto. Mbinu za uteuzi wa kimaksudi na kuelekezwa zilitumiwa kuteua sampuli ya wasailiwa wa kike kumi na wanne wenye umri wa miaka katika 30-70 walioshirikishwa katika utafiti. Vikundi lengwa viwili viliundwa kutokana na sampuli hiyo. Kila kimoja kilijumlisha wasailiwa sita, cha kwanza kilikuwa na wasailiwa wenye umri kati ya miaka 50-60 na cha pili kilikuwa na wasailiwa wenye umri kati ya 30-48. Wasailiwa wawili wenye umri zaidi ya 64 walishirikishwa katika mahojiano ya kina. Bembelezi 20 zilikusanywa katika vikundi lengwa vya mjadala na sita zikateuliwa kimaksudi kwa misingi ya maudhui zilizobeba ili kutafitiwa. Matokeo ya utafiti huu yalionyesha kwamba, maudhui ya bembelezi za wanawake Watikuu hulenga si watoto tu, bali watu mbalimbali katika jamii hiyo. Lililodhihirika ni kwamba wanawake Watikuu hutumia bembelezi kama jukwaa la mawasiliano. Wanapowabembeleza watoto kwa kuwaimbia, huwa wanayatoa yaliyo mioyoni mwao kwa nyimbo hizo. Maneno Muhimu: maudhui, bembelezi, wanawake watikuu. http://www.editoncpublishing.org/ http://www.editoncpublishing.org/ mailto:akakalina2016@gmail.com DOI: 10.51317/ecjkisw.v3i1.205 Volume: 03 Issue: 01 | Feb-2021| Received: 24.01.2021; Accepted 28.01.2021; Published on 28.02.2021 at www.editoncpublishing.org Akaka, L., et al., Editon Cons. J. Kiswahili., Double –Blind Peer Reviewed Journal 212 © 2021, Editon Consortium Publishing | This work is licensed under a Creative Commons Attribution-Non Commercial-Share Alike 4.0 International License. | Website: www.editoncpublishing.org Editon Consortium Journal of Kiswahili (ECJKISW) ISSN: 2663-9289 UTANGULIZI Bembelezi ni wimbo rahisi, wa kutuliza, wenye mdundo na urudiaji ambao huimbiwa mtoto kumbembeleza (Gunes na Gunes, 2012). Makala hii itashughulikia bembelezi zinazoimbwa na wanawake Watikuu, wenyeji wa Kisiwa cha Faza kilicho ndani ya Kisiwa cha Pate, Mashariki mwa Kisiwa cha Amu. Utamaduni wa bembelezi ni mkongwe katika jamii ya Watikuu, kwa mujibu wa wasailiwa, zimekuwepo kwa zaidi ya karne nane zilizopita, akina mama na nyanya zao waliimbiwa pia. Kwa hakika asili ya nyimbo hizi katika jamii hii wala kujua wakati zilipoanza, tarehe wanazodhani kwamba zilianza ni za kukisia tu. Katika jamii nyingi, bembelezi zinajulikana kuwa nyimbo za watoto ambazo zina maudhui mepesi na urudiaji mwingi wa maudhui hayo; huenda ndiyo watafiti wengi wamekipuuza kitanzu hiki cha watoto. Hata hivyo bembelezi za Watikuu zinaonyesha kinyume cha mambo, ujumbe uliyomo ni tata, uchunguzi unaonyesha zina ujumbe anuwai wenye uzito ambao mtoto hawezi kuelewa. Makala hii itajadili maudhui ya baadhi ya bembelezi hizi ili kuyaweka wazi. Msingi wa Nadharia Utafiti uliongozwa na nadharia ya ethinografia ya mawasiliano kwa mujibu wa Saville-Troike (2003) na mhimili wa “yaliyomo katika ujumbe” ukatumiwa kujadili maudhui katika bembelezi za Watikuu. Troike (hj) anasema muundo wa ujumbe na yaliyomo katika ujumbe ni mambo yanayohusiana, na hivyo vipengele viwili mara nyingi haviwezi kutenganishwa. Yaliyomo katika ujumbe kwa mujibu wa Hymes na Gumperz (1972) yanarejelea matendo ya kimawasiliano na maana ambayo inawasilishwa. Troike (hj) anasema ili yaliyomo katika ujumbe yawasilishwe na kufasiriwa kikamilifu, habari za awali kuhusu mada inayozungumziwa ni muhimu sana. Matokeo ya Utafiti Ilibainika wazi kuwa bembelezi za Watikuu zina maudhui anuwai yasiyolenga tu watoto bali watu wengineo katika jamii. Wanawake Watikuu huzitumia kama jukwaa la kujieleza, kutoa wosia kwa mabinti zao, kukemea waume zao na kadhalika. Kutokana na maudhui yaliyomo, uhusiano katika ya mlezi na watu mbalimbali katika jamii pia hubainika. Unafiki Katika bembelezi ya unafiki, mlezi amesalitiwa na rafiki yake wa kike wa karibu sana. Uchungu na hasira alizo nazo moyoni kufuatia tendo ambalo rafiki yake alimtendea ni nyingi kiasi kwamba huenda akimkabili ana kwa ana, kutatokea vita, na ili kuzuia jambo kama hilo, anatoa lalama zake kwa bembelezi ambayo dhamira yake kuu machoni mwa jamii ni kumwimbia mtoto kwa nia ya kumbembeleza lakini ndani mna ujumbe ufuatao: Howa nchocho howa x2 Nyamaza mtoto nyamaza Nilikufanya rafiki kakupa siri za ndani Nilikufanya rafiki nikakupa siri zangu binafsi Kisha kakufanya wanda kakutia matoni Kisha nikakutengenezea wanja nikakutia machoni Karama uwe ni simba hunila ndani kwa ndani Kumbe wewe ni simba unanila kisirisiri Wanawake Waswahili wakipendana hupendana kama ndugu hata ule urafiki ukavuka mipaka ya urafiki na wakawa zaidi ya ndugu. Katika ubeti wa kwanza hapo juu, mlezi anaanza mshororo wa kwanza kwa kumnyamazisha mtoto kisha anamwambia rafiki yake waliokuwa wakifanya wakiwa marafiki. Katika huo http://www.editoncpublishing.org/ http://www.editoncpublishing.org/ DOI: Volume: 03 Issue: 01 | Feb-2021| Received: 24.01.2021; Accepted 28.01.2021; Published on 28.02.2021 at www.editoncpublishing.org Akaka, L., et al., Editon Cons. J. Kiswahili., Double –Blind Peer Reviewed Journal 213 © 2021, Editon Consortium Publishing | This work is licensed under a Creative Commons Attribution-Non Commercial-Share Alike 4.0 International License. | Website: www.editoncpublishing.org Editon Consortium Journal of Kiswahili (ECJKISW) ISSN: 2663-9289 urafiki wao, bila rafikiye kujua, akawa kama gawadi wa bintiye na kumpa rafiki wa kiume; gawadi kwa maana ya mtu anayemtongozea mwingine msichana au mvulana akawa ni yeye wa kuwakutanisha. Baada ya mama yake huyo binti kugundua hila ambayo rafiki yake wa karibu alimfanyia, alitunga bembelezi akimlaumu rafiki yake na kutoa uchungu aliokuwa nao kufuatia jambo hilo. Katika mshororo wa pili wa ubeti wa kwanza wa bembelezi ya unafiki anaeleza vile alivyomwamini rafiki yake, akampa siri zake za ndani na kumtia wanja machoni kumbe rafikiye alikuwa akimla ndani kwa ndani. Ule undani wa mlezi ambao rafiki alikuja kuujua ndio aliutumia kumfanyia kitendo ambacho sasa kimemletea kilio. Katika mshororo wa kwanza ufuatao wa ubeti wa pili, mlezi baada ya kugundua yaliyomfika bintiye analalamika kwa kusema: Karatasi ya maini mwenye kusoma ni nyani? Karatasi ya majini atakayeisoma ni nani? Karatasi iliyoloa maji, atakayeisoma ni nani? Karatasi ambayo ina maandishi ikianguka majini wino utatapakaa na maandishi yatatatiza kusoma. Mlezi anamlinganisha bintiye na karatasi iliyoanguka majini ikaloa maji, maandishi yake hayawezi kusomeka kwa kuwa wino uliotumiwa kuandika umetapakaa. Alonitakia imi ni mwanangu Asumani Aliyeniletea balaa mimi ni mwanangu Asumani Kuchukua va ahera kuvaeta duniani Kuchukua waliofariki kuwaleta duniani Kama ilivyotajwa awali, bembelezi moja inaweza kubeba ujumbe anuwai; katika bembelezi ya unafiki, mlezi alianza kwa ujumbe mkuu wa unafiki aliofanyiwa na rafikiye, kisha akaanza kulalamika kumhusu mwanawe wa kiume, Asumani. Asumani alioa na mke wake akawa hasikilizani na mama yake. Mlezi anasema kwamba, mtoto wake Asumani amemletea balaa, mke wa Asumani huchukua wa ahera na kuwaleta duniani; yaani ni kama huwafufua waliokufa kwa kuwataja. Mama anasema mke wa Asumani akianza kumtusi, huwatusi pamoja na jamaa zake waliofariki zamani. Kua mwanangu Rukiya nikusomeshe skuli Kuwa mkubwa mwanangu Rukiya nikuelimishe Nikufundishe ubembe uhadaliye vavuli Nikufundishe unyumba, umtunze mume Ni nyani afungudhieyeo nami nichie kufuli Ni nani aliyefungua nifunge Katika hiyo mishororo mitatu ya mwisho, ujumbe unabadilika na kuwa wa wosia. Mlezi anamhimiza mtoto kukua, Sarv (2013) anaonyesha pia kwamba ujumbe katika bembelezi za kiEstonia uliwahimiza watoto kukua; Sarv (hj) anasema bembelezi zilizoimbwa sana ni za kumrai mtoto kukua haraka ili asaidie na kazi za shamba, kuchunga mifugo, kwenda mtoni, kutunda matunda na mengineyo. Mlezi anamwambia mwanawe Rukiya kwamba akue ampeleke skuli; isitoshe amfundishe jinsi ya kuishi na mume, amfundishe unyumba na ndoa, jinsi atakavyomtunza mumewe. Katika mshororo wa mwisho anamuuliza mtoto aliyemfungua ili amtie kufuli. Hili ni fumbo alilomfumbia akimuuliza iwapo kuna mtu aliyekwishamjua kimwili kwa hivyo anasema atazitia kufuli sehemu zake za siri pasitokee mwingine akazifungua. Kwa jicho la kiuhakiki hili ni onyo tu kwa mtoto kwamba ajitunze hadi atakapoolewa, asije mtu akamharibu ubikira. Maneno kama haya kwa mtoto asiyejua lolote kuhusu mapenzi http://www.editoncpublishing.org/ http://www.editoncpublishing.org/ DOI: Volume: 03 Issue: 01 | Feb-2021| Received: 24.01.2021; Accepted 28.01.2021; Published on 28.02.2021 at www.editoncpublishing.org Akaka, L., et al., Editon Cons. J. Kiswahili., Double –Blind Peer Reviewed Journal 214 © 2021, Editon Consortium Publishing | This work is licensed under a Creative Commons Attribution-Non Commercial-Share Alike 4.0 International License. | Website: www.editoncpublishing.org Editon Consortium Journal of Kiswahili (ECJKISW) ISSN: 2663-9289 yanatilia shaka iwapo kweli ni huyu mtoto anaambiwa haya au kuna mwingine anakusudiwa kuyasikia. Mizozo ya Kifamilia Katika jamii nyingi ulimwenguni, mizozo ya kifamilia huwa ni jambo la kawaida kwa sababu ya utangamano na mlahaka walio nao; watu wanaishi pamoja hawana budi kutoelewana kwa jambo moja au jingine na hatimaye wakapatana. Bryant na wengineo (2001) wanasema mizozo kati ya mavyaa na mkazamwana huzua chuki na mihemko na kuathiri ndoa kwa njia hasi. Jambo hili si jipya katika jamii za kiafrika kama inavyodhihirika katika fasihi zao iwe simulizi au andishi; mwanamke akishaolewa katika familia, kuna wale humpenda na kuna wale huwa na mtazamo hasi kumhusu, na hali hii inaweza kusababisha kutoelewana. Bembelezi ya mizozo ya kifamilia inaonyesha hali ifuatayo ya mambo: Howa nchoncho howa x2 Nyamaza mtoto nyamaza Yana Tima Tumu alinichukana Jana Tima Tumu alinitukana Hakuchusaza vazee kwa vana Hakutubakisha wazee kwa watoto Asojua ruli simpe maana Asiyejua fumbo usimfumbulie Katika huo ubeti wa kwanza wa bembelezi ya mizozo ya kifamilia, mlezi anasema Tima Tumu alimtukana. Tima Tumu ni jina la mtu lakini si la mavyaa wake, amembandika jina hilo ili ujumbe anaopitisha usiwe wa moja kwa moja. Tima Tumu (mavyaa) aliwatukana wakubwa kwa wadogo hakuna mmoja aliyebakishwa katika matusi yale, wote walijumuishwa pamoja. Mwimbaji ni mkaza mwana wa Tima Tumu; mtu na mavyaa wake hawaelewani. Kutoelewana hutokea kati ya mavyaa na mkaza mwana kwa sababu za kiuchumi, mama yake mume humwona mke wa mwanawe kama ambaye alikuja kupunguza pato lake. Senti alizokuwa akipata yeye peke yake sasa zinagawanywa katika ya mke na mama na hili husababisha uadui kati yao. Mishororo miwili ya kwanza inazungumza kuhusu vile mavyaa alimtukana mkaza mwanawe pamoja na watu wa kwao, wadogo kwa wakubwa. Katika mshororo wa tatu, mlezi anasema kwamba asiyejua maana ya fumbo asifumbuliwe. Ahamad usinene maneno machafu Ahamad usiseme maneno machafu Kama huyasadiki kavulize vatu Kama huyaamini kawaulize watu Usiveke nyama katika siafu Usiweke nyama katika siafu Mshororo wa kwanza wa ubeti wa pili unaakisi mlezi aliyechoka na vitendo vya mavyaa wake akamwambia mtoto wake Ahamad asichukue tabia ya nyanya yake ya kuwasema watu kwa ubaya. Mackinlay na Baker (2005) wanasema bembelezi ziliakisi simanzi, hofu na lalama za akina mama na kuimba hisia hizi katika mazingira yasiyo na vitisho vyovyote na kwa undani wa moyo kuliwaruhusu kutoa hisia zilizogubika mioyo yao na kuitakasa. Mara nyingi walipata faraja kwa watoto wao ingawa hawakuelewa uzito wa hisia walizokuwa nazo; isitoshe walitumia wakati huo kuwashauri, kuwaonya na kuwaelimisha watoto kutokana na tajriba zao binafsi. Katika mshororo wa pili, mlezi anamhimiza mtoto kwenda kuuliza watu iwapo anayomwambia ni ya kweli au la; iwapo haamini kuwa kweli nyanya yake, alimfanyia http://www.editoncpublishing.org/ http://www.editoncpublishing.org/ DOI: Volume: 03 Issue: 01 | Feb-2021| Received: 24.01.2021; Accepted 28.01.2021; Published on 28.02.2021 at www.editoncpublishing.org Akaka, L., et al., Editon Cons. J. Kiswahili., Double –Blind Peer Reviewed Journal 215 © 2021, Editon Consortium Publishing | This work is licensed under a Creative Commons Attribution-Non Commercial-Share Alike 4.0 International License. | Website: www.editoncpublishing.org Editon Consortium Journal of Kiswahili (ECJKISW) ISSN: 2663-9289 mama yake anayomwambia. Katika mshororo wa mwisho, anamshauri kwamba asije akawa na tabia ya kuweka nyama katika siafu; pande la nyama likiwekwa kwenye siafu, watalivamia na kulila lote. Hilo ni fumbo kwa maana ya kuwa kwenye watu wengi, usimseme mwenzio kwa kuwa yuko mmoja atakayetoka pale na kumrudishia aliyesemwa maneno hayo. Katika hii bembelezi ya mizozo ya kifamilia, mlezi anajaribu kumshauri mtoto kwa kumpigia mfano halisi unaofanyika katika familia wakati huo ili kumtahadharisha kuepuka tabia kama hiyo. Mwana Ahamad sikiza lambwao Mwana Hamad sikiza linalosemwa Usikize ngoma sura ziliavo Usikize ngoma sura ziliavyo Mahaba matamu ataka pumbao Mapenzi ni matamu yanataka pumbao Mlezi anamwambia mtoto kusikiliza maneno yanayosemwa kumhusu, jinsi maneno tofauti yanavyosemwa; anatumia fumbo, usikize ngoma sura ziliavyo kwa maana ya kuwa asikilize vile mipigo ya ngoma inavyobadilika. Mlezi anafumba fumbo katika mshororo huo, analinganisha kumsema anakomsema mavyaa na mpigo wa kila aina wa ngoma. Kwa sababu ya maneno mengi ambayo mavyaa alisema kumhusu mkaza mwana wake, anamzomea katika mshororo wa mwisho wa ubeti huu kwamba, hata ingawa mavyaa alisema yote ambayo alisema, haondoki pale. Mkazamwana katika hii bembelezi anapigania nafasi yake kama mke wa mumewe, anamjibu mavyaa kwa kumwambia amempumbaza mume wake kwa mahaba kwa sababu mahaba huwa matamu mtu akipumbazwa; kwa hivyo hakuna vile mumewe atamuacha, mavyaa apende asipende wataendelea kuishi pamoja. Katika bembelezi ya mizozo ya kifamilia, mlezi anaeleza kuhusu kutoelewana kwake na mavyaa huku akimshauri mtoto kwa kumpigia mfano wa kisa hicho. Mwimbaji wa bembelezi hii alikuwa akitoa hisia zake kuhusu uhusiano wake na mavyaa, kilio chake dhidi ya mama yake mumewe. Umbeya Katika mshororo wa kwanza wa ubeti wa kwanza wa bembelezi ya umbeya, mlezi anaanza kwa kumtuliza mtoto anyamaze, kisha katika mshororo wa pili, anasema kwamba, kuna chungu kilichoandaliwa na kila siku kinatokota. Howa nchocho, howa x2 Nyamaza mtoto nyamaza Kuna chungu kiandisiwa huchokocha siku zote Kuna chungu kiliandaliwa na hutokota siku zote Mwishiza mai jabia na kuni makoko yote Mmemaliza maji katika tangi na makoko yote ya kuni Mja hupanga kupata huva hataki akose Mtu hupanga kupata huwa hataki kukosa Mlezi anatoa taswira ya hali ya mambo ilivyo kwa kuturegesha kwenye mazingira ya mekoni. Ni kawaida chungu kinapotokota mekoni, kinachopikwa hukauka maji na ikabidi yaongezwe ili vipikwavyo visije vikaungua. Katika mshororo wa pili, anaeleza vile chungu kilizidi kuongezwa maji hadi yakaisha katika jabia; isitoshe kuni nazo pia ziliisha kwa kuongezwa mekoni ili kuchochea moto uwake zaidi. Mlezi anatoa taswira ya vile umbeya ulivyozidi, watu wakatoa habari nyingi kumhusu haswa za uongo hata wakakosa la kumsema; bembelezi ya umbeya inaakisi jamii ambamo watu hushughulika na maisha ya kibinafsi ya wenzao. http://www.editoncpublishing.org/ http://www.editoncpublishing.org/ DOI: Volume: 03 Issue: 01 | Feb-2021| Received: 24.01.2021; Accepted 28.01.2021; Published on 28.02.2021 at www.editoncpublishing.org Akaka, L., et al., Editon Cons. J. Kiswahili., Double –Blind Peer Reviewed Journal 216 © 2021, Editon Consortium Publishing | This work is licensed under a Creative Commons Attribution-Non Commercial-Share Alike 4.0 International License. | Website: www.editoncpublishing.org Editon Consortium Journal of Kiswahili (ECJKISW) ISSN: 2663-9289 Muifanyiza wajuzi hapo siasa hamuziisi Mmejifanya wajuaji siasa hamuachi Chungu mukiandisecho hulalamika vapishi Chungu mlichoandaa hufanya wapishi walalamike Mutazidi kutotea ama mutaveka iti Mtazidi kukichochea au mtakiweka chini Katika ubeti wa pili, mlezi anasema, wanaomsengenya wanajifanya wajuaji, siasa haziwaishi. Wakati wote watu wakisema maneno wasiyoelewa, wasiyoweza kuthibitisha au wasiokuwa na uhakika nayo, huwa wanasemwa kwamba wanapiga siasa. Mlezi anasema kwamba, wapishi hulalamika kwa sababu ya chungu kilichoandaliwa; hili ni fumbo linalomaanisha kwamba, wanaosikiliza huo umbeya unaondelea kuenea hulalamika kuhusu wanayosema wambeya. Husema kwamba yanayosemwa hayafai kwa sababu ni kuingilia ndoa ya watu kwa kusema habari wasizojua kuihusu. Katika mshororo wa tatu, anataka kujua iwapo watazidi kuchochea umbeya au wataacha. Kwenenda si kukimbia kusimama si kusona Kutembea si kukimbia na kusimama si kupumzika Vatu va madarasani vana himaya ya kusoma Walimu wa dini wana hekima kutokana na masomo yao Upanga uko nundoni vachu huchezea goma Upanga uko ndani ya nyundo watu hucheza ngoma Katika ubeti huu, mlezi katika mshororo wa kwanza anasema kutembea si kukimbia na kusimama si kupumzika. Hapa mlezi anaonekana kuwajibu wanaomsengenya; ingawa hakutaja kamwe mambo yaliyosemwa juu yake lakini kwa fasiri ya mtafiti, inaonekana wambeya walikuwa wakisema vile mambo yake hayaendi vizuri. Katika mshororo wa pili anawasifu walimu wa dini. Mwimbaji alienda kwa walimu wa msikitini kutaka ushauri wao kuhusu mambo ambayo watu walikuwa wakisema. Anasema kwamba wana hekima kwa kuwa wamesoma mambo ya kidini. Katika mshororo wa tatu, anatumia fumbo, kueleza vile umbeya huo umekuwa kama densi kwa wasikilizaji. Watikuu wana ngoma ya kiutamaduni inayoitwa upanga; ngoma ya upanga ni mchezo au densi inayochezwa na wanaume kwa panga. Hufundisha wanaume namna ya kupigana kwa upanga huku wakijikinga kutokana na adui wasije wakajeruhiwa. Mlezi analinganisha umbeya unaoendelea kumhusu na mchezo huo wa ngoma ya upanga. Wosia Jukumu la kuusia watoto wa kike Uswahilini ni la akina mama na mashangazi. Wazazi wa mtoto wa kike huwa roho juujuu wanapomlea mtoto wa kike kwa sababu huwa na wasiwasi kwani huenda akailetea familia aibu kwa kupata mimba kabla ya ndoa, kuavya mimba au ubikira ukaharibiwa na arusi ikakosa kujibu atakapofikia wakati wa kuolewa. Haya ni mambo yanayoweza kuwakosesha akina mama usingizi kwa sababu huleta aibu ya kudumu kwa familia, familia zingine zinapowashauri binti zao, huyo msichana anakuwa ni wa kurejelewa kila wakati kama mfano mbaya usiostahili kuigwa. Kwa kuwa mojawapo ya vipengele vya utamaduni wa Watikuu ni utunzi na utongoaji wa mashairi, kuna wale ambao hutunga mashairi kuhusu aibu hizo na hali hii inaweza kuitatiza familia husika kimawazo. Bembelezi ya wosia ina ushauri kwa mtoto wa kike ambaye amefikia umri wa kuolewa. http://www.editoncpublishing.org/ http://www.editoncpublishing.org/ DOI: Volume: 03 Issue: 01 | Feb-2021| Received: 24.01.2021; Accepted 28.01.2021; Published on 28.02.2021 at www.editoncpublishing.org Akaka, L., et al., Editon Cons. J. Kiswahili., Double –Blind Peer Reviewed Journal 217 © 2021, Editon Consortium Publishing | This work is licensed under a Creative Commons Attribution-Non Commercial-Share Alike 4.0 International License. | Website: www.editoncpublishing.org Editon Consortium Journal of Kiswahili (ECJKISW) ISSN: 2663-9289 Howa nchoncho howa x2 Nyamaza mtoto nyamaza Bamba ni kitu muhimu kwa kusi na kaskazi Paa ni kitu muhimu wakati wa pepo za kusi na kaskazi Na nyumba pia hudumu hupungua nyingi kazi Na ndoa hudumu kwa kupungua kwa kazi Waume hujifahamu mambo yote ni wazazi Waume wajue wazazi walifanya kazi nyingi kwa wake zao Hatimaye katika mshororo wa pili, anaanza kuusifu uzuri wa bamba kwamba ni muhimu kwa kusi na kaskazi; bamba hapa kwa maana ya mume huku kusi na kaskazi zikirejelea raha na shida. Watikuu huezeka paa za nyumba zao kwa kutumia mabati au makuti kutegemea hali ya kiuchumi ya familia; hivyo hili linaeleza matumizi ya neno bamba, neno hilo limetumiwa badala ya makuti ili kuonyesha hali ya kudumu ya ndoa, kando na makuti ambayo muda wake wa kudumu ni mfupi. Isitoshe maneno kusi na kaskazi hutumiwa katika mazingira ya pwani ambapo pepo hizo huvuma; msimu wa kusi huwa na baridi nyingi, mvua na samaki wengi baharini ilhali msimu wa kaskazi wenye jua kali, kiangazi na upungufu wa samaki baharini. Mlezi anamuusia mwanawe kwamba mume ni mtu muhimu kwa raha na shida kwa kuwa humsitiri mkewe kwa hali zote, kuwa na mume, kwa mujibu wa mlezi huyo ni kama kufichwa uchi au kuwa na nyumba ambapo unaweza kujikinga kutokana na hali mbaya za anga. Katika mshororo wa tatu, anaambiwa kwamba, nyumba hudumu na kazi kupungua. Msichana akiwa kwao kabla ya ndoa, hutumikishwa na wazazi wake. Mama humpangia kazi kila wakati, bila kumpumzisha, ndiyo njia moja ya kuhakikisha kuwa yule binti hana nafasi ya kuondoka nyumbani, jambo ambalo huwasaidia kumtunza. Kwa hivyo katika kipande cha pili cha mshororo wa tatu, anamwambia, kazi zilizokuwa nyingi hupungua, maadamu mwenyewe sasa yuko kwake, atajipangia kazi zake mwenyewe. Kipande cha kwanza cha mshororo wa tatu, kinasema na nyumba pia hudumu; neno nyumba limetumiwa kwa maana ya ndoa. Mama anamweleza mwanawe kwamba, ndoa hudumu, mume akifanya majukumu yake. Katika mshororo wa mwisho mlezi anamkumbusha mwanawe kwamba, mumewe atafahamu kwamba, alifanya kazi kubwa kwake kama mama hata bintiye akawa mke. Ubeti ufuatao wa bembelezi ya wosia unatoa ushauri wa ndoa kwa mtoto: Howa nchocho howa x2 Nyamaza mtoto nyamaza x2 Bamba ndilo la kufaa kwa mvua na hata jua Paa litakufaa kwa mvua na jua Wala sikate tamaa kwa Mungu lolote huwa Usikate tamaa kwa Mungu lolote lawezekana Nyumba ni yako haswa kwa mtu atakutowa Hakuna anayeweza kukuondoa katika nyumba yako Katika ubeti wa pili, mlezi anamwambia mtoto kwamba mume atamfaa kwa raha na dhiki. Mwanamume ni kama paa, humhifadhi mwanamke katika hali yoyote maishani vile ambavyo paa la bamba huwahifadhi wenye nyumba katika misimu ya mvua na jua. Mlezi anashauri iwapo kuna dhiki yoyote asikate tamaa, awe mwenye subira na ukakamavu, Mungu atamwepushia; anamsisitizia kuwa ndoa yake ni kama nyumba, hakuna anayeweza kumuondoa mle lakini akienda kuishi kwa mtu atamtoa, kupata ndoa ni kama kupata nyumba haswa kwa mwanamke. Katika jamii za kiafrika, ndoa humithilishwa na nyumba; msichana akiolewa, husemwa kwamba amepata nyumba. http://www.editoncpublishing.org/ http://www.editoncpublishing.org/ DOI: Volume: 03 Issue: 01 | Feb-2021| Received: 24.01.2021; Accepted 28.01.2021; Published on 28.02.2021 at www.editoncpublishing.org Akaka, L., et al., Editon Cons. J. Kiswahili., Double –Blind Peer Reviewed Journal 218 © 2021, Editon Consortium Publishing | This work is licensed under a Creative Commons Attribution-Non Commercial-Share Alike 4.0 International License. | Website: www.editoncpublishing.org Editon Consortium Journal of Kiswahili (ECJKISW) ISSN: 2663-9289 Nyamaza Mtoto Bembelezi ya nyamaza mtoto ni mfano halisi wa bembelezi jinsi zinavyojulikana katika tamaduni nyingi ulimwenguni; urahisi wa lugha na wepesi wa ujumbe. Mlezi anazungumza na mtoto usiku, anamnyamazisha ili sauti yake isitoke nje. Howa nchocho howa x2 Nyamaza mtoto nyamaza Silie usiku ndia zina vachu Usilie usiku njia zina watu Zina vaswalina na vachavo Mungu Zina wasio mcha Mungu na wachao Mungu Mame mwanangu niombea Mungu siku ya utungu Mamangu aliniombea siku ya kujifungua Katika mshororo wa kwanza wa ubeti wa kwanza, mlezi anaanza kwa kumwambia mtoto anyamaze. Hatimaye katika mshororo wa pili ambao unaendelezwa na mshororo wa tatu anamwambia asilie kwa kuwa njia zina watu; wachawi, mashetani na majini, pia zina waswalina na wamchao Mungu. Imani na itikadi za Watikuu zinadhihirika katika bembelezi katika mshororo huo; Troike (2003) anahoji kuna uhusiano kati ya muundo na ujumbe uliomo ndani ya lugha na imani, amali na mahitaji yaliyomo ndani ya utamaduni wa wazawa wa lugha. Mshororo huo unadhihirisha imani waliyo nayo kuhusu usiku kwa uhusiano na kilio cha watoto. Howa nchoncho, howa x2 Nyamaza mtoto nyamaza Silie mwana kilio cha daima Usilie mtoto kilio cha muda mrefu Hunitoa mchilinga nami michilinga sina Unanitoa mitulinga nami sina mitulinga Sina urithi mwanangu na imi mwana bibie mbwainya Sina urithi wa kukupa mwanangu nyanyako ni kama mama yako Katika mshororo wa kwanza wa huu ubeti wa pili, mama anamweleza mtoto asilie kilio cha daima. Inaonekana kuwa mtoto alikuwa hatulii, mama akasumbuka usiku huo kwa sababu ya kero za mtoto. Katika mshororo wa pili, anamwambia vile usumbufu wake ulivyomkondesha; mlezi anasema vile kilio cha mtoto humtoa mitulinga. Mackinlay na Baker (2005) wanasema akina mama walitumia bembelezi kueleza dhiki zao, kueleza mtoto walivyojitolea kuona kwamba anapata faraja huku wao mwenyewe akiikosa. Katika mshororo wa mwisho, Mama anamwambia mwanawe kwamba, kwa mumewe yeye hana urithi, lakini kwao anao na urithi wake ni kama wa mwanawe; kile ambacho mama yake au bibi ya mtoto atamrithisha, ndicho naye atamrithisha. Howa nchoncho, howa x2 Nyamaza mtoto nyamaza Ukenda hondeni tukuwa bori na daba Ukienda shambani beba chombo na debe Na vunga vako taani japokuwa ni kibaba Na unga wako mfukoni hata ukiwa mchache Usiatie ruhuni yatakuvua mahaba Usiyatie rohoni mapenzi yatakuuwa http://www.editoncpublishing.org/ http://www.editoncpublishing.org/ DOI: Volume: 03 Issue: 01 | Feb-2021| Received: 24.01.2021; Accepted 28.01.2021; Published on 28.02.2021 at www.editoncpublishing.org Akaka, L., et al., Editon Cons. J. Kiswahili., Double –Blind Peer Reviewed Journal 219 © 2021, Editon Consortium Publishing | This work is licensed under a Creative Commons Attribution-Non Commercial-Share Alike 4.0 International License. | Website: www.editoncpublishing.org Editon Consortium Journal of Kiswahili (ECJKISW) ISSN: 2663-9289 Katika huu ubeti wa mwisho, kama ilivyo desturi ya wanawake Watikuu kushauri watoto, mlezi anampa mtoto ushauri utakaomfaa akiwa mkubwa. Matarajio ya mlezi kwa mtoto ni kuwa atakua na kuanza kufanya shughuli ambazo kila mtu hufanya maishani. Kwa hivyo anamshauri akienda shambani abebe bori (kibuyu kilichotengenezwa kutokana na boga la malenge lililokaushwa) na daba (kibuyu cha bamba). Katika mshororo wa kwanza mtoto anashauriwa kubeba maji, debe litabeba maji kisha atumie bori kuyanywa. Katika mshororo wa pili anaambiwa autie unga mfukoni na aubebe pia hata ingawa ni kidogo. Mazungumzo kama hayo ya mama kwa mtoto yanapatikana katika bembelezi za Estonia pia; Sarv (2013) alisema bembelezi za kiEstonia zilianza kwa maneno ambayo yalichochea usingizi na kubembeleza mtoto. Hatimaye mlezi alimwamrisha mtoto kukua ili amsaidie mama kazi. Bembelezi za waYoruba nazo ziliwaadilisha watoto na kuwaeleza jinsi maadili waliyotarajiwa kuwa nayo katika hatua mbalimbali za ukuaji wao Akinyemi (2003) Kwa hivyo hali ya kutumia bembelezi kueleza matarajio ambayo walezi walikuwa nayo dhidi ya watoto si jambo geni, lilifanywa katika tamaduni tofauti. Mshororo wa mwisho unazungumzia jambo tofauti kabisa ambalo halina uhusiano na maneno aliyosema awali. Mlezi anajua kwamba, mtoto atakuja kukabiliana na mambo ya mapenzi akikua mkubwa. Kwa hivyo anamshauri mtoto kuwa, asitie mapenzi rohoni, asipende kupita kiasi kwa sababu mapenzi huua, hususan akiwa ndiye atakayependa sana kuliko vile atakavyopendwa. Maudhui ya mapenzi yalijitokeza katika bembelezi za waMakunduchi ambazo zilitafitiwa na Haji (2017); katika bembelezi hizo, wanaume kwa wanawake walitahadharishwa kuepuka kudanganya watu kwamba wanawapenda kwa sababu mapenzi ya upande mmoja huleta madhara kwa anayependa. Mshororo wa mwisho unazungumzia jambo tofauti kabisa ambalo halina uhusiano na maneno aliyosema awali. Mlezi anajua kwamba, mtoto atakuja kukabiliana na mambo ya mapenzi akikua mkubwa. Kwa hivyo anamshauri mtoto kuwa, asitie mapenzi rohoni, asipende kupita kiasi kwa sababu mapenzi huua, hususan akiwa ndiye atakayependa sana kuliko vile atakavyopendwa. Majuto Bembelezi ya majuto imebeba ujumbe wa majuto unaowasilishwa kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Troike (2003) anasema huu ni mkakati wa mawasiliano ambao hutumika katika tamaduni mbalimbali ili kutohusisha linalosemwa na mtu yeyote. Baadhi ya bembelezi za Watikuu zina sifa ya kuwa na ujumbe uliomzidi mtoto, ujumbe tata. Hali hii inaonekana pia katika bembelezi za jamii nyinginezo za Waswahili kama vile waMakunduchi; Haji (2017) anatoa mifano ya bembelezi za waMakunduchi ambazo zilibeba ujumbe tata, vilevile bembelezi za waPemba vile alivyobaini Ali (2013). Howa nchoncho howa x2 Nyamaza mtoto nyamaza Huliya mwana huliya Hulia mtoto hulia Husaliwa na mayuto Hubaki akijuta Ungaufuta ushingo Ungeuondoa uchungu Mshororo wa kwanza unaanza kwa kumnyamazisha mtoto, mlezi anasema nyamaza, nyamaza. Kisha katika mshororo wa pili anasema kwa kurudia kuwa mtoto hulia na kusema kuwa baada ya mtoto kulia, husaliwa na http://www.editoncpublishing.org/ http://www.editoncpublishing.org/ DOI: Volume: 03 Issue: 01 | Feb-2021| Received: 24.01.2021; Accepted 28.01.2021; Published on 28.02.2021 at www.editoncpublishing.org Akaka, L., et al., Editon Cons. J. Kiswahili., Double –Blind Peer Reviewed Journal 220 © 2021, Editon Consortium Publishing | This work is licensed under a Creative Commons Attribution-Non Commercial-Share Alike 4.0 International License. | Website: www.editoncpublishing.org Editon Consortium Journal of Kiswahili (ECJKISW) ISSN: 2663-9289 majuto, anachojutia mtoto hakisemwi katika bembelezi. Kinajulikana na mlezi na huenda “mtoto” anayerejelewa si huyo anayebembelezwa. Ujumbe katika mshororo wa mwisho wa ubeti huu unaendelezwa katika mshororo wa kwanza wa ubeti unaofuatia isitoshe maudhui yanabadilika. Mtoto aliyekuwa akibembelezwa sasa anaambiwa hata akiifuta sumu, kovu litabaki tu. Maneno haya yanasemewa mtu kando na mtoto; mshale huwa na sumu na ukimdunga mtu kisha utolewe, utaacha kovu, lile kovu litakuwa kumbukumbu ya ule uchungu aliohisi mtu alipodungwa. Mlezi aliimba kuhusu mume aliyemwacha mke wake akamchukua mwanamke mwingine, mara alipogundua kuwa mke wake alikuwa bora kumliko huyo aliyemchukua, alijuta na kurudi kwa mke wake. Kwa bahati mbaya, akapata kwamba mke wake alikuwa tayari ashaolewa na mume mwingine. Hilo lilimtia uchungu ikawa ni kama alidungwa na mshale uliokuwa na sumu; na akabaki akifuta ushingo au sumu kwa hivyo aliyekuwa mume wake ataishi na hilo kovu la kumkosa. Howa nchoncho howa x2 Nyamaza mtoto nyamaza Unacho chembe unacho Unao uchungu unao Alhamdulilahi kwa Mola nishukurie Alhamdulilahi namshukuru Mola Leo hupemba mwanangu Leo nambembeleza mwanangu Nduza vanisaidie Ndugu zangu wanisaidie Huu ubeti wa pili unaendeleza ujumbe ulio katika ubeti wa kwanza. Mlezi anazidi kumwambia aliyekuwa mume wake kwamba anacho chembe; hilo lina maana kwamba anao uchungu, uchungu wake unatokana na hali ya kwamba, baada ya kuondoka katika ndoa kwa sababu ya mwanamke wa nje, baada ya mambo kumharibikia, alitaka kumrudia mke wake lakini akakataa, hiyo ndiyo sababu ya uchungu wake. Mlezi anamshukuru Mungu kwa sababu ya vile mambo yalivyomwendea aliyekuwa mume wake na kusema siku hiyo anambembeleza mtoto wake. Huyu mwanawe anayesema kwamba anabembeleza, kimafumbo ni mume aliyemuoa baada ya kutoka kwa mume wa kwanza. Anawaita ndugu zake wamsaidie kusherehekea furaha yake; ni kawaida watu kujuta kwa mambo waliyofanya punde tu wanapotambua makosa yao. Mahitimisho na Mapendekezo Kutokana na matokeo ya mjadala wa data, imebainika wazi kwamba, bembelezi za Watikuu hubeba ujumbe mbalimbali; wanawake Watikuu hutumia bembelezi kama jukwaa la kutakasa hisia na kusemezana na watu waliowakosea katika jamii. Kwa hivyo kosa alilokosewa mtu ndilo huamua ujumbe ambao bembelezi itabeba; hata hivyo kuna bembelezi zilizopokezwa pia au zile ambazo ni za kimapokeo lakini maudhui yakafaraguliwa ili kufungamana na hali aliyomo mlezi. Taswira nyingine iliyojitokeza katika bembelezi hizi ni kwamba, mlezi hubuni maudhui kutegemea hali aliyomo au iliyompata. Kulingana na wasailiwa, hadhira ya bembelezi si watoto peke yao; kuna baadhi ya nyimbo ambazo mtoto hufaidi kutokana na melodia yake huku maudhui yakilenga hadhira tofauti. Bembelezi za Watikuu hutumiwa na wanawake katika jamii hiyo kama jukwaa la suluhu ya amani ya kutatua mizozo kati yao; kama alivyosema Chiraghdin (1973) katika Abdalla (2012) kwamba, “Na mtu akiwa na dhiki ya moyo, hapana njia bora kuliko kulitoa alilonalo moyoni. Na kwa Mswahili, njia nzuri zaidi ni ya kutongoa kwa mashairi na nyimbo, akiwa ajua.” http://www.editoncpublishing.org/ http://www.editoncpublishing.org/ DOI: Volume: 03 Issue: 01 | Feb-2021| Received: 24.01.2021; Accepted 28.01.2021; Published on 28.02.2021 at www.editoncpublishing.org Akaka, L., et al., Editon Cons. J. Kiswahili., Double –Blind Peer Reviewed Journal 221 © 2021, Editon Consortium Publishing | This work is licensed under a Creative Commons Attribution-Non Commercial-Share Alike 4.0 International License. | Website: www.editoncpublishing.org Editon Consortium Journal of Kiswahili (ECJKISW) ISSN: 2663-9289 Utafiti zaidi ufanyiwe kitanzu cha bembelezi katika jamii zingine za Uswahilini na nje ya jamii hizi kwa kuwa utafiti huu umeonyesha kwamba kitanzu hiki cha watoto kingali hai, hakijafa. Isitoshe, wingi wa tafiti za bembelezi zilizotangulia hususan za kimagharibi zilifanya sana utafiti wa kimaabara na utafiti wa vipengele vya kimuziki, ujumbe na muundo ukashughulikiwa kwa kiasi kidogo. Barani Afrika hususan katika mataifa ya Afrika magharibi na kusini, watafiti walishughulikia swala la maudhui na muundo ilhali katika Afrika Mashariki na haswa nchini Kenya, bembelezi hazijafanyiwa haki ya utafiti. Watafiti wanapendekeza kuwa, bembelezi za jamii zote nchini Kenya zitafitiwe kwa ujumla wake wote katika vipengele vya kimuundo, kimaudhui, kimawasiliano na kiutamaduni. Watafiti wanapendekeza utafiti zaidi ufanyiwe bembelezi hizi kwa mtazamo wa kianthropolojia ili kutambua zaidi utamaduni wa jamii hii kama unavyodhihirika katika nyimbo zenyewe. Utafiti zaidi ambao pia utachukua mtazamo wa kimawasiliano unapendekezwa kwa sababu matokeo ya utafiti huu yanaonyesha kwamba bembelezi hizi ni chombo cha mawasiliano. Wanawake Watikuu huzitumia kama jukwaa la kujieleza na kusemezana miongoni mwao. Ni jukwaa la suluhisho la amani la mizozo baina yao. Kwa hivyo utafiti zaidi unaweza kufanywa ili kuchunguza hali hii. Ikiwezekana, utafiti wa kimaabara ufanyiwe sio tu bembelezi za Watikuu bali za jamii za kiAfrika zote kama ule uliofanyiwa bembelezi za kimagharibi. Utafiti wa kimaabara utasaidia katika kuchunguza athari zake kwa ukuaji wa watoto kisaikolojia na ujifunzaji lugha na muziki na matokeo ya utafiti kama huo utawafaa sana walimu wa shule za chekechea pamoja na waundaji mitalaa ya shule za chekechea ambao husisitiza sana kuwa watoto waelimishwe kupitia kwa nyimbo mapema katika maisha. Uchunguzi ufanywe ili kubaini iwapo ujumbe katika bembelezi hizi huchangia kukuza maadili ya mtoto kwa njia chanya au hasi hususan ikikumbukwa kwamba, nyingi zimejaa maneno ya ugomvi na lalama za akina mama dhidi ya waume zao. Hisia za huzuni na mtamauko unaombatana na nyimbo hizi akina mama wanapoziimba pia huenda zinawaathiri watoto kihisia, pengine hili ni jambo la kufanyia utafiti zaidi. Bembelezi za Watikuu huimbwa na wanawake, kwa hivyo utamaduni umezitenga kama nyimbo za wanawake. Watafiti wanapendekeza bembelezi hizi zitafitiwe zaidi kwa mtazamo huu ili kuchunguza jinsi wanawake wanavyotumia lugha katika nyimbo zao, jinsi wanawake wanavyohusiana na wanaume katika nyimbo hizi, wanavyohusiana kimamlaka kati yao na wanaume, na mahusiano ya wanawake wenyewe kwa wenyewe yanayojitokeza katika bembelezi hizi, na jinsi wanawake wanavyobuni fasihi simulizi zao kutokana na mwono- ulimwengu wao. MAREJELEO Abdalla, A. (2012). Sauti ya Dhiki. Nairobi: Oxford University Press. Akinyemi, A. (2003). 'Yoruba Oral Literature: A Source of Indigenous Education for Children' Katika Akin Oyatede (ed) In Journal of African Cultural Studies. Vol (16)2, Pp 161-179. Ali, S.A. (2013), “Athari za Mtindo katika Kuibua Maudhui: Mifano kutoka Bembelezi za Pemba.” Unpublished M.A (Kiswahili) Thesis. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. http://www.editoncpublishing.org/ http://www.editoncpublishing.org/ DOI: Volume: 03 Issue: 01 | Feb-2021| Received: 24.01.2021; Accepted 28.01.2021; Published on 28.02.2021 at www.editoncpublishing.org Akaka, L., et al., Editon Cons. J. Kiswahili., Double –Blind Peer Reviewed Journal 222 © 2021, Editon Consortium Publishing | This work is licensed under a Creative Commons Attribution-Non Commercial-Share Alike 4.0 International License. | Website: www.editoncpublishing.org Editon Consortium Journal of Kiswahili (ECJKISW) ISSN: 2663-9289 Bryant, C.M. etal. (2001). “The Influence of In-laws on Change in Marital Success”. In Journal of Marriage and Family, 63, Pp 614- 626. Gunes, H. na Gunes, N. (2012). “The Effects of Lullabies on Children”. In International Journal of Business and Social Science. Vol. 3, No. 7 Pp 316 – 321. Haji, Z.R. (2017). “Kuchunguza Dhamira na Fani katika Nyimbo Bembelezi za Watoto: Mifano kutoka Makunduchi.” UnPublished M.A. (Kiswahili) Thesis, Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania. Hymes, D.H. na Gumperz, J.J. (1972). “Models of the Interaction of Language and Social Life.” In Gumperz J.J. and Hymes, D. (eds) Directions in Sociolinguistics: Ethnography of Communication, Pp 35- 71. New York: Holt, Rinehart and Winston. Mackinlay, E. & Baker, F. (2005). “Nurturing Herself, Nurturing Her Baby: Creating Positive Experiences for First-time Mothers through Lullaby Singing,” Women and Music, 9, Pp 69- 89. Sarv, Mari (2013). “Traditional Estonian Lullabies: Tentative Overview.” In Laineste, L. Brzozowska, D. na Chlopicki, W. (eds). Creativity and Tradition in Cultural Communication. Volume 2: Perspectives on National and Regional Identity. Tartu: Elm Schorlarly Press. Pp 161- 176. Saville-Troike, M. (2003). Ethnography of Communication: An Introduction. 3rdEdition. London: Blackwell Publishing. http://www.editoncpublishing.org/ http://www.editoncpublishing.org/